Serikali za Ethiopia na Djibouti zimekubaliana kujenga bomba la kusafirishia gesi asilia, lenye urefu wa kilometa 767 kati ya nchi hizo mbili.
Wizara ya Madini na Petroli ya Ethiopia ilisema mwishoni mwa wiki kuwa kampuni ya Kichina ya Poly-GCL Petroleum Group Holdings Limited (PolyGCL) ndiyo iliyopewa kazi ya kujenga bomba hilo la gesi asilia.
Mradi huo umeleta matumaini kwa nchi zote mbili kuongeza mapato yao ya fedha za kigeni mara bomba hilo litakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.
Imeelezwa kuwa mipango ya serikali ya Ethiopia ni kuzalisha Dola za Marekani bilioni moja kila mwaka, kutokana na uchimbaji wa gesi asilia na mafuta ghafi.
Taarifa zinasema kuwa bomba hilo litakalojengwa mwaka huu na Kampuni ya Poly-GCL, litawezesha kusafirishwa kwa gesi hiyo asilia kutoka Ethiopia ambayo haina mlango wa bahari hadi katika bandari za Djibouti katika kipindi cha miaka miwili.
Kilometa 700 za bomba hilo litakuwa katika ardhi ya Ethiopia, wakati kilometa zingine 67 zilizobaki zitakuwa katika ardhi ya Djibouti.
Imeelezwa kuwa hivi karibuni, Kampuni ya Poly-GCL iligundua kuwepo kwa futi za ujazo kati ya trilioni saba hadi nane za gesi asilia nchini Ethiopia.
Poly-GCL ni kampuni ya nishati inayohusika na utafutaji, uhifadhi, usafirishaji, usindikaji pamoja na masoko ya biashara ya bidhaa hiyo.
Comments