Makala

Rubani Susan Mashibe: Jinsi alivyoweza kutimiza ndoto yake

0
Susan Mashibe
Susan Mashibe

Kila mtu ana ndoto yake katika maisha, huu ni muongozo ambao kama utaufuata basi ni rahisi kufikia kwenye matamanio yako au sehemu ambayo unahitaji kufika.

Pamoja na milima na mabonde, haipaswi kukata tamaa katika safari ya kwenda kufikia ndoto zako za kimaisha badala yake ni kusimama imara.

Susan Mashibe ni mwanamke ambaye anaeleza kuwa hakuwahi kukata tamaa kufikia ndoto yake ambayo aliiota akiwa na miaka mine, historia yake ya maisha anaieleza mbele ya wasichana ili iwe kama somo kwao, wasikate tamaa bali wawe imara kuhakikisha wanafikia katika ndoto zao.

Kama alivyojitambulisha mbele ya mkutano wa mabinti ulioandaliwa na Taasisi ya Msichana anasema alizaliwa mwaka 1973 mkoani Kigoma, wazazi wake walikua huko kikazi lakini yeye ni wenyeji wa Mwanza. Suzan ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto sita.

Ndoto yake ya kuwa rubani mwanamke barani Afrika anasema ilianza akiwa na umri wa miaka minne wakati wazazi wake wakisafiri na ndege kutoka Kigoma kwenda jijini Dar es Salaam.

“Sisi tulikua tunabaki na bibi lakini wadogo zangu wawili wanasafiri na wazazi wangu, tulipokua uwanjani mimi naangalia ndege, wakapanda na ndege ikaruka…iliniuma sana nikafikiria kama nikijua kurusha ile ndege wazazi wangu hawataniacha tena,” anasema.

Tangu hapo nia, dhamira na mawazo na ndoto yake ndipo ilipozaliwa baada ya kuachwa na wazazi wake waliopanda ndege. Susan anasema alisoma shule za serikali, mwaka 1981 alianza darasa la kwanza Shule ya Msingi Nyanza na kuhitimu darasa la saba mwaka 19887 kisha alijiunga na Sekondari ya Pamba na kuhitimu mwaka 1991.

Safari yote hiyo ya kielimu Susan anasema kuwa aliendelea kusafiri na ndoto yake ya kuendesha ndege. “Nilikua nafanya vizuri sana darasani lakini ni kwa sababu baba alikua akifurahia sana maendeleo yangu na kila ninapoleta matokeo nyumbani baba alininunulia zawadi ilinifanya niendelee kujitahidi ili nipate zawadi ya nguo na viatu vipya,” anasema.

Susan anasema alipomaliza kidato cha nne alichaguliwa kwenda kusomea ualimu lakini baba yake alimuuliza anataka kusomea nini yeye akamuambia anataka kutimiza ndoto yake ya kuwa rubani.

Anasema dada na mama yake mdogo walikua wakiishi Marekani ilibidi wazazi wake wafanye mpango aende kusomea huko. “Maisha yetu yalikuwa ya kawaida sana hivyo tulipata tu nauli nikaondoka Tanzania, nilipofika huko nilianza kufanya kazi ya kutunza wazee na wenye ulemavu,” anasema Susan.

Soma pia:  Nigeria yasogeza mbele uchaguzi

Mwanadada huyo anasema baada ya kupata fedha kidogo na ndugu zake hao kumchangia alikwenda kujiunga na Chuo cha Masuala ya Ndege (aviation) moja kwa moja lakini alipofika huko akabaini kuwa kutokujua kingereza kwa ufasaha ilikuwa changamoto hivyo asingeweza kazi hiyo.

“Nikagundua na kiingereza changu hiki nisingeweza kwa sababu kule uwanja ni mkubwa mawasiliano ni ya haraka haraka na kiingereza kinachoeleweka sio kwa maneno ya kutafuta,ilibidi nijifunze kwanza lugha hasa kwenye kuzungumza,” anasema.

Kwa mujibu wa Susan alishauriwa kusoma uhandisi wa kutengeneza ndege kwanza wakati akijifunza kiingereza, ufundi ulihusisha vitendo vya ufundi pekee kwa sabubu urubani ilihitaji kufahamu lugha kwa ufasaha kwa sababu ya mawasiliano wakati wote.

Alisoma Shahada kwa miaka miwili kupata uwezo wa kutengeneza ndege na akafanya mtihani wa Federal Aviation Administration (FAA) na kufaulu vizuri.

“Nilihitimu ingawa haikua lengo langu mimi nilikua nikisoma kozi hiyo wakati nasubiri lugha ipande ili nirushe ndege lakini ikawa kama baraka nikapata mambo mawili yaani ufundi wa ndege na pia urubani,”anasema.

Suzan anawasisitiza na kuwahamasiha wasichana kutimiza na kufuata ndoto zao. Anasema alifanya kazi sana, usiku na mchana ili kufanikisha ndoto yake. “Yaani nilikua nalala hoi asubuhi naenda darasani na usingizi, nafanya kazi hospitali kuosha wagonjwa, ilibidi nibadili saa za kulala nalala mchana,” anasema.

Anasema alipokuwa mhandisi, mshahara ulipanda na alipata ufadhili wa masomo kwa nusu ada alipoanza kusomea urubani na kuhitimu mwaka 2003 na alisomea Aviation Management baada ya hapo alirudi Tanzania.

Suzan anasema alirudi kwa sababu hakua na kazi nyingine ya kudumu baada ya makampuni mengi ya ndege kushindwa kufanyakazi kwa sababu ya tukio la ugaidi la Septemba 11 nchini Marekani.

Alipofika Tanzania alijaribu kuomba kazi kampuni mbalimbali za ndege lakini hakupata ajira huku wengine wakimwambia kiwango chake cha elimu kiko juu sana. “Wakati niko Marekani ndege ikiletwa kwetu tunaifungua kila kitu kuikagua zinakaa pale hata miezi mitatu, hata kama kuna kutu, hapa walikuwa hawafanyi hivyo kwa hiyo waliona niko juu sana,” anasema.

Anasema aliamua kurudi Marekani lakini siku moja bahati ilimuangukia kwa njia nyingine, alikuja mteja na ndege aina ya Jet kuangalia kama ina matatizo kabla haijanunuliwa, bosi wake alimkutanisha na mteja huyo ili aweze kumkagulia kwa kuwa huyo mteja alikua anatoka Afrika Kusini.

“Mabosi wangu walipoondoka mimi nikajiongeza nikazungumza na wale wateja kwamba wanaonaje nikawafanyia kazi wakiwa wanakuja Afrika hata kama sitapata fedha nyingi lakini nibaki kwenye fani yangu, waliomba wasifu wake (CV) nilipowapa wakahoji kwa nini nataka kumfanyia mtu kazi kwa elimu yangu hiyo?” anasema.

Soma pia:  Ethiopia na Djibouti kujenga bomba la gesi

Susan anasema wale wateja walimuambia huwa wanapata shida sana wanapokuja Afrika na ndege binafsi hasa Tanzania kwa sababu mifumo ya kuhudumia watu wanaokuja na ndege binafsi ni migumu.

“Wote niliowauliza changamoto yao ilikuwa moja, wanasema huku malipo ni lazima kulipa fedha na huduma haipo pamoja na kuzunguka, basi nikapanga nikianza kazi hii nitaanza kutumia kwa malipo ya kadi maalum (credit card) na sio fedha taslimu hasa katika kuwatafutia mafuta ya ndege, chakula na vibali,” anasema.

Susan anasema wale watu walimshauri arudi Tanzania akaanzishe kampuni ya kuunganisha huduma zote zinazohitajika kwa watu wanaokuja na ndege binafsi ili wazipate sehemu moja kama vile mafuta, chakula, kupata vibali vya kutua na kuruka.

“Kwa sababu nilikua ni mhandisi na rubani ilikua ni rahisi kwangu najua rubani anataka nini na ndege inataka nini nikaanza kupata mwanga, nikaanza kufuatilia wote walionieleza changamoto ni hiyo huduma hizo kuwa mbalimbali na pia malipo,” anasema na anaongeza kuwa wakati huo pia alikuwa mwanamke mwafrika mhandisi peke yake.

Anasema mwaka 2003 aliamua kurudi Tanzania kutazama fursa nyingine za maisha ingawa bado alitamani kurusha ndege.

Susan anasema alipoanza kazi hiyo ilisaidia pia kuondoa mianya ya upotevu wa fedha za serikali kwani walikua wakilipa moja kwa moja kwa hundi kwenda kwenye akaunti za serikali jambo ambalo lilianza kumletea uhasama na baadhi ya watumishi wa serikali walikua wanajipatia fedha kwa mianya hiyo.

Anasema sifa yake ilisambaa kwamba kuna kampuni fulani inatoa huduma zote, wateja waliokua wakija nchini walimuomba kufanya huduma hiyo hata katika nchi nyingine za Afrika.

“Kwa hiyo kwa sasa mimi ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika wa huduma za ndege binafsi, huwa naenda kuelimisha watu wanaokuja Afrika watapata wapi huduma zote hizo,” anasema Mwanadada huyu anasema kwa sasa anatoa huduma pia kwa wageni wanaokuja na ndege za kawaida za abiria lakini wakifika nchini wanahitaji ndege za kukodi kama wanahitaji huduma za safari binafsi.

Susan anasema mwanzoni alianza kama majaribio lakini baadaye akabaini kuwa kuna watu wengi wanahitaji huduma hiyo hivyo akaamua kujikita kutoa huduma.

Anasema aliweza kutengeneza uwanja wa ndege wa Kilimanjaro kuwa maarufu kwani ndege binafsi zilianza kutua wakati awali zilikuwa zikitua za abiria na kwenda kukaa nchi jirani Hata hivyo anasema kwa sasa kuna kampuni nyingine kama nne ambazo zinafanya kazi kama anayofanya yeye kwa hiyo biashara sasa imekuwa ya ushindani “Wengine hasa wako kwenye ndege za abiria lakini sisi sasa tumejikita kwa ndege za watu binafsi, kama anakuja Oprah, sisi tunaunganisha huduma zote tunasubiri tu uamuzi wa mteja anataka kuondoka saa ngapi, kuwachukulia nyaraka zote za safari ambako ni nchi chache sana Afrika wanafanya ninachofanya mimi,” anasema.

Soma pia:  Mgomo Makerere bado moto

Kampuni ya Susan inayoitwa VIA Aviation iko nchi nne, Tanzania, Senegal, Rwanda na Mali.

Anasema kampuni kupitia kampuni yake hiyo ameweza kufundisha vijana kufanya service kwenye ndege na kuwa wana vifaa ambavyo wanahudumia vitu vidogo vidogo.

Kampuni yake sasa ina watu 19 lakini pia wana kampuni nyingine ambayo ameungana na watu wengine hiyo inahudumia bara zima la Afrika.

Susan anasema kwa sasa urubani hafanyi sana ila amebaki anafanya mara chache kama ‘hobby’ na pia kuna huduma anafanya kwenye ndege za wateja wake kama vile huduma ya kuongeza upepo unapopungua au oksijeni.

Anasema kuna huduma nyingine katika ukarabati wa ndege anaweza kufanya lakini hafanyi kwa sababu inahitaji vifaa na pia watu wa kutosha wenye ujuzi na sio kufanya peke yake.

“Mimi nilifanya kazi ya uhandishi miaka minne lakini hadi mwaka wangu wa pili ndio nilianza kabisa kuachiwa kwamba unaweza kufanya mwenyewe lakini mwanzoni unafanya kwa usimamizi,” anasema na anaongeza kuwa kuna huduma ambazo huwa wanaomba makampuni mengine hapa nchini na baadhi ya nchi kwenda kusaidia kufanya ukarabati wa ndege Anasema pia ana kampuni nyingine ambayo kazi yake ni kuwatafutia wageni vibali vya ndege wale ambao wanapita katika bara zima la Afrika ambayo inachangia sh bilioni mbili kwa mwaka.

Susan anasema ndoto yake ni kumiliki helikopta kwani anataka kujifunza kurusha ili aweze kusafirisha wateja wake wakija.

Kurusha ndege

Mwaka 2000 anasema alirusha ndege kwa mara ya kwanza peke yake na anaongeza kuwa hatakuja kuisahau siku hiyo.

“Unatoka unapewa nenda umbali fulani, unaambiwa zunguka umbali huu kisha rudi, unafanya lakini hii unakuwa na mwalimu au msimamizi, lakini baadaye unapewa ramani unaambiwa nenda mwenyewe, unaenda, unaongea na mnara wa mawasiliano baadaye unaambiwa uende mbali,”anasema.

Comments

Comments are closed.

More in Makala