Mchuano mkali unaendelea kutokea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England baada ya Manchester City kuiondoa kieleni Liverpool, ambayo ilishikilia kwa kipindi kirefu uongozi wa ligi hiyo.
Manchester City imefikisha pointi 62 sawa na Liverpool, lakini ina idadi kubwa ya mabao licha ya kuwa mbele kwa mchezo mmoja baada ya kucheza mechi 26, huku Liverpool ikiwa nyuma pungufu kwa mechi moja.
Vinara hao wapya ambao pia ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England baada ya kuifunga Everton kwa mabao 2-0 na kushika usukani huo wa msimamo wa Ligi Kuu ya England. Hatahivyo, Manchester City itakuwa na kibarua kigumu kesho Jumapili wakati itakapokutana na Chelsea katika mchezo wa ligi hiyo na endapo itashinda, basi itaendelea kujiweka vizuri katika kilele cha ligi hiyo.
Kocha wa Man City Pep Guardiola, ambaye ni kocha wa Manchester City pamoja na timu yake kupewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika msimu huu wa ligi, lakini yeye anasema kuwa kuna timu kadhaa zinaweza kutwaa taji hilo.
Kikosi cha kocha Jurgen Klopp kingeweza kufikia pointi saba kama wangeifunga Leicester wiki iliyopita, lakini sare ya bao 1-1 na baadae kulazimishwa sare nyingine na West Ham Jumatatu, kuliitia doa timu hiyo. Sare hizo mbili zimeiwezesha Man City kurejea katika mbio, na kuifunga Arsenal 3-1 Jumapili iliyopita kumeiwezesha timu hiyo kurejea kileleni na kuitia hofu Liverpool kama inaweza kutwaa taji hilo.
Hata hivyo, baada ya wiki mbaya kwa Man City, ambayo ilianza kwa timu hiyo kufungwa 2-1 Jumanne kutoka kwa timu ya Newcastle iliyopo katika hatari ya kuteremka daraja, Guardiola anaamini kuwa bado kuna mchuano mkali kuelekea mwishoni mwa msimu.
“Siku tatu au nne zilizopita, tayari tumeshafanya mambo, na Liverpool kama ligi ingemalizika kipindi hicho, basi ingekuwa bingwa. Lakini sasa ndio tuko katika nafasi kubwa na tunatarajia kuongoza ligi. Tunajitahidi kuwa watulivu,“ alisema Guardiola kabla ya Man City kucheza dhidi ya Everton Jumatano usiku. “Itashtua sana na mambo yatakuwa mazito kwa timu kuweza kushinda kila mchezo. Washindani na wale ambao sio washindani wana uwezo wa mbinu za kuleta mataizo.”
Mbio za Ubingwa
Man City ilishinda taji msimu uliopita ikiweka rekodi katika Ligi Kuu kwa kufunga mabao 100, lakini Guardiola anaona kuwa utawala huo ni wakawaida katika soka la Uingereza. “Naweza kusema kuwa hii ni aina ya soka la England, hali ndivyo ilivyo,” alisema.
“Kitu ambacho sio cha kawaida ni kile kilichotokea msimu uliopita, ambako tulishinda mechi 18 mfululizo, pamoja na pointi 100 na kuwaacha wengine mbali (timu iliyokuwa katika nafasi ya pili).
“Kitu kilichotokea sasa ni cha kawaida, kila mchezo ni mgumu, ambapo unaweza kushinda au kufungwa kila mchezo, kwa sababu kila timu inajihusisha katika kuwania taji, au kutaka nafasi ya kucheza Ulaya, au kuendelea kubaki katika Ligi Kuu.” Guardiola pia aliongeza kusema kuwa itakuwa ni jambo la kupuuzi endapo utaziondoa katika mbio za ubingwa Tottenham, Chelsea au hata Manchester United iliyopo katika nafasi ya tano.
Spurs kabla ya mchezo wa Jumatano wa Man City, walikuwa pointi mbili nyuma ya mabingwa hao watetezi. “Hilo ni swali kwenu,” Guardiola alisema. “Kamwe sijawahi kusema Tottenham hawamo katika mbio za ubingwa.
Chelsea, pia sijawahi kusema kuwa nao hawapo. United, Na kama wataendelea kwenda na mwendo huu, basi United nao watakuwa katika mbio hizo.
“Watu sasa wanaona msimamo ulivyo, na wanaona ya kwanza, ya pili au ya tatu, na huwezi kuangalia zaidi ya hapo. Chelsea inaweza kushinda mfululizo michezo michache na kuwa mshindani wa kuwania taji. Kuna pointi 39 za kuwania. Kila timu iko tayari kupata pointi.”
Kocha wa Everton, Marco Silva yuko katika shinikizo kubwa baada ya kufungwa Jumatano, licha ya kushinda mechi tatu kati ya 12 za ligi zilizopita, kutolewa katika raundi ya nne ya Kombe la FA dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza ya Millwall.
Lakini Guardiola anaamini kuwa Toffees (Everton) wanatakiwa kuwa wa tulivu na kumpa muda zaidi kocha wao huyo Mreno ili aweze kuiwezesha kufanya vizuri zaidi huko mbele.
“Watu hawajui kabisa ugumu wa kutengeneza timu, inachukua muda,“ alisema Guardiola. “Endapo wanamuamini kocha huyo wa Everton, wanatakiwa kusonga naye mbele. Itachukua muda, lakini itategemea na wao wenyewe.”
Comments