Michezo

TP – Mazembe yahitimisha safari ya Simba CAF Champion League

0
Mazembe Simba CAF
Simba vs Mazembe

Safari ya wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), Simba SC, kufikia mwisho kwa kuondoshwa mashindanoni wakikubali kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa TP Mazembe.

Mtanange huo wa mkondo wa pili wa robo fainali ya michuano hiyo, uliopigwa mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ulikuwa wa aina yake kutokana na matukio na soka lililotandazwa katika dakika 90 za kibabe na timu zote mbili.

Simba waliendeleza rekodi mbaya ya michezo ya ugenini kwa kupoteza mechi ya tano mtawalia, huku wakifanikiwa kufunga bao moja na kuvunja jinamizi la rekodi mbaya ya kutopata bao katika viwanja vya ugenini kwenye mechi za hatua ya makundi na mtoa.

Matokeo ya suluhu ya robo fainali ya kwanza iliyopigwa wiki moja iliyopita jijini Dar es Salaam yaliufanya mchezo huo wa jana kuwa wa kiufundi zaidi, kwani ulikuwa wazi kwa kila timu kuutumia vema kutinga nusu fainali.

Mpambano huo wa jasho na damu kwa kila timu, ulianza kwa kasi kwa wenyeji kupeleka shambulizi kali dakika ya kwanza lililozaa kona iliyopigwa na kuokolewa na mabeki wa simba.

Soma pia:  Simba SC kuandaa bajeti ya Usajili

Simba walitumia nafasi hiyo kuanzisha shambulizi la kushitukiza kupitia kwa Mzamiru Yassin akaipenyeza kwa kiungo Harunaa Niyonzima aliyepiga pasi ndefu katikati mwa uwanja na kumkuta Emmanuel Okwi, katikati ya mabeki wawili na kuwapindua kuiandikia Simba bao la kuongoza dakika ya pili.

Baada ya bao hilo wenyeji walionekana kutoka mchezoni, lakini taratibu walianza kurejea huku Mnyama akizimiliki dakika 20 za kipindi cha kwanza kwa soka mujarabu.

Mambo yalianza kubadilika dakika ya 22, TP Mazembe walianza kutumia winga zao hasa Meshack Elia aliyeanza kucheza winga ya kulia dhidi ya Mohamed Hussein mara kadhaa alishindwa kupenya na kubadilisha upande.

Kunako dakika hiyo Elia aliambaambaa na mpira kusini mashariki mwa uwanja na kumtikisa beki wa kulia wa Wekundu wa Msimbazi, Zana Coulibaly na kufanikiwa kupata kona.

Pigo la mpira huo lilizaa matunda kwa makosa ya safu ya ulinzi ya Simba, ambayo Kabaso Chongo aliyatumia vema na kuisawazishia TP Mazembe, bao ambalo liliwatoa Simba mchezoni, huku wapinzani wao wakionekana kurejea na kuliteka pambano kwa dakika kadhaa.

Soma pia:  Mambo yaiva Simba vs Al Ahly Taifa kesho

Mazembe kupitia kwa Elia aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa Simba aliwanyanyua mashabiki wao waliokuwa wamefurika kwenye uwanja wa nyumbani kwa kupachika bao la pili mara baada ya kutumia vema makosa ya Coulibaly.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyoonekana kucheza vibaya sana licha ya makosa yaliyofanywa na mabeki wa Simba, huku mlinda mlango wao Aishi Manula akiwa nyota kwa upande wao katika dakika hizo 45.

Kipindi cha pili timu zote zilirejea kwa kasi huku Simba wakifanya badadiliko ya kuwatoa Juuko Murshid na Mzamiru Yassin nafasi zao zikichukuliwa na Clatous Chama na Meddie Kagere.

Mpango wa Kocha Patrick Aussems wa Simba kutaka kushambulia katika kipindi hicho ulishindwa kuzaa matunda kwa aina ya soka walilorejea nalo TP Mazembe, kwa kutawala dimba la kati huku wakitanua uwanja wakiishambulia Simba.

Dakika ya 61 alikuwa ni Mputu aliyewanyanyua kwa shangwe mashabiki kwa kupachika bao muja-rabu yakiwa ni makossa yale yale ya safu ya ulinzi na kuimarisha uongozi wa Mazembe kwa mabao 3-1.

Soma pia:  Simba yampa mkataba wa miaka miwili Kagere

Aussems aliendelea kujaribu kutafuta upenyo wa kupindua matokeo kwa kumtoa Emmanuel Okwi na nafasi yake kuchukuliwa na kijana machachari Rashid Juma dakika ya 70.

Siku iliendelea kuwa bora kwa wenyeji kwa kucheza soka safi katika kipindi cha pili, huku Elia akiwa mwiba mkali akiwapindua mabeki wa Simba kulia na kushoto sambamba na Muleka aliyekuwa na mchezo bora hapo jana.

Muleka alihitimisha kalamu ya mabao kwa kuifungia Mazembe bao la akiwaapindua mabeki wa Simba kutoka kaskazini mashariki mwa uwanja na kuachia kombora kali lililotikisa nyavu za Simba kwa mara nyingine.

Simba walijaribu kupambana kutafuta mabao, lakini mlima ulikuwa mkubwa kwao kwani Mazembe waalikuwa imara kulinda lango lao.

Katika dakika 10 za mwisho, Chama na Coulibaly walijaribu mashuti makali yaliyolenga lango pasi na mafanikio ya kupata bao.

Dakia 90 za mtanange huo zilimalizika kwa Mazembe kutinga nusu fainali kibabe wakiwafurumusha Simba mabao 4-1.

Comments

Comments are closed.

More in Michezo