Umoja wa Afrika (AU) umependekeza ufanyike mkutano wa kimataifa kujaribu kutatua mgogoro wa Libya. Taarifa iliyotolewa juzi imesema umoja huo wenye wanachama 55 utapenda kufanya mkutano huo wa usuluhishi Julai mwaka huu kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa.
Malengo ya mkutano huo ni kutengeneza mfumo kwa ajili ya uchaguzi Oktoba mwaka huu Tume ya AU, Umoja wa Mataifa pamoja na Serikali ya Libya zimeombwa kuchukua hatua zote muhimu kwa ajili ya uchaguzi huo wa rais na wabunge.
Libya iliingia katika mgogoro wa kisiasa na machafuko tangu kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi alipopinduliwa mwaka 2011. Nchi hiyo inakabiliwa na mvutano baina ya makundi mbalimbali.
Yapo mawili yanayokinzana yaliyounda serikali huku kila kundi likitaka kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo. Kundi moja linalotambuliwa na Umoja wa Mataifa lina makao yake Tripoli wakati lingine makao makuu yake ni katika mji wa Tobruk.
Wakati huohuo yako makundi mengine yenye silaha ambayo yote yamekuwa yakitaka kushika madaraka na utajiri wa nchi hiyo.
Comments