China na Umoja wa Afrika (AU) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao kwa masuala ya amani na usalama kupitia mpango wa Amani na Usalama wa China na Afrika.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika walikuwa na mazungumzo na Waziri Msadizi wa Mambo ya Nje wa China, Chen Xiaodong (pichani), kuhusu utekelezaji makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa Afrika na China wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) Septemba, 2018.
Mawaziri hao wa Afrika walikutana mjini Addis Ababa kwa ajili ya kikao cha kawaida cha 34 cha Baraza la Utendaji Februari 7 hadi 8, 2019. Kupitia Mkutano wa FOCAC, China ilikubali kujenga jumuiya ya karibu na Afrika kwa ajili ya mustakabali wao wa pamoja wa baadaye.
Chen alisema mambo yaliyokubaliwa kwenye mkutano huo ni kuimarishwa kwa ushirikiano kuhusu amani na usalama wa China na Afrika.
“China inatumaini mazungumzo haya yataleta ushirikiano katika kufikiri na kutenda kati ya pande hizi mbili, tushaurinane namna gani tutatekeleza mpango wa amani na usalama na kuweka nguvu katika ushirikiano wa amani na usalama wa China na Afrika,”alisema Chen.
Waziri huyo Msaidizi wa Mambo ya Nje wa China, alisema ingawa hali inazidi kuimarika, lakini hatari na changamoto zinazoikabili amani na usalama wa Afrika haziwezi kupuuzwa.
Comments