Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amemuagiza Katibu Tawala mkoa kuwachukulia hatua wakuu wa idara wote waliosababisha kuibuka kwa hoja za ukaguzi wa hesabu za Serikali katika halmashauri mkoani humo.
Aliyasema hayo jana wilayani Nzega kwenye baraza maalumu la madiwani wa halmashauri ya wilaya hizo la kujadili na kujibu hoja za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoshia Juni 30, mwaka huu.
Mwanri alimtaka RAS kuanza kuwachukulia hatua kwa kuwaondoa wakuu wote wa idara ambao wamekwenda kinyume cha taratibu na hivyo kuzisababishia halmashauri zao kuwa na hoja.
Alisema hoja nyingi ambazo zimeibuka zinasababishwa na wakati mwengine manunuzi yaliyofanyika kukosa viambatanisho kama vile stakabadhi za malipo yaliyofanyika na nyingine kutofuata taratibu za manunuzi jambo ambalo linaloelekea katika matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mwanri alisema kuwa Serikali haiwezi kuvumulia mtendaji au mkuu yoyote wa idara ambaye hana nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na hivyo kusababisha hasara ambayo inapelekea baadhi ya miradi kutokamilika.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa mwezi mmoja hoja zote zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali zinapata majibu ikiwa ni kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kusababishia Halmashauri ya Wilaya ya Nzega hasara.
Aliwagiza Katibu Tawala Mkoa kuhakikisha hasara halmashauri hiyo kuwasiliana na TAMISEMI hata kama wamehama warudishwe waje wajibu hoja zinazowakabili.
Katika hatua nyingine aliitaka halmashauri hiyo kuja na utaratibu wa kulipa madeni ikiwa ni pamoja na ile asilimia 10 kwajili ya vijana, wanawake na walemavu.
Alisema kuwa, utaratibu huo ni lazima pia uonyeshe jinsi pesa hizo zitakavyorejeshwa ili watu wengine waweze kukopa. Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Msalika Robert Makungu aliwataka watendaji mbalimbali kuwa na uzalendo wakati wa utelekezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha kila wanachokifanya kinazingatia maslahi mapana ya umma.
Alisema, moyo wa kizalendo ndio utasaidia kukwepa dosari mbalimbali zinazoibua hoja kutoka kwa Mkaguzi wa hesabu za serikali.
Aidha, aliwataka masiwani na watendaji kufanya kazi kwa ushirikiano katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri kwajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Aliwasilisha taarifa ya CAG inayohusu Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Mkoa wa Tabora, Mohamed Msangi alisema, katika mwaka wa fedha 2016/17 zilitolewa hoja 40 ambapo kati ya hizo 14 zimefungwa na hoja 26 zimesalia.
Comments