Top Stories

Coca-Cola kusafisha Coco Beach mwaka mzima

0
Coca-Cola kusafisha Coco Beach
Coco Beach

Kampuni ya Coca-Cola Kwanza imeingia makubaliano na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kusafi sha fukwe zilizopo kwenye manispaa hiyo na imeanza na ufukwe wa Coco.

Akizungumza Dar es Salaam juzi Mkurugenzi Mkuu wa Coca-Cola Kwanza, Basil Gadzios alisema makubaliano hayo ni mradi wa majaribio wa mwaka mmoja ya kusafisha ufukwe huo na iwapo utafanikiwa wataingia makubaliano na halmashauri nyingine nchini kote.

Katika makubaliano hayo ambayo yanakwenda sambamba na kampeni yake ya ‘Mchanga Pekee’, wameajiri wanawake na vijana kwa ajili ya kufanya usafi huo kwa kuwapa vifaa na fedha, ambapo watakuwa wanaondoa plastiki na uchafu mwingine na kubakisha mchanga pekee kwenye ufukwe huo.

“Kama sehemu ya kampeni hii ya Mchanga pekee, Coca-Cola Kwanza pia imejikita kukusanya chupa za plastiki 10,000 kwa kila mwezi. Katika kampeni hii Coca-Cola Kwanza itazinunua chupa kutoka kwa wananchi kupitia safari za utembeleaji wa jamii kwenye maeneo yao, Wananchi watakusanya chupa na kampuni kuzinunua kwa bei iliyopangwa kwa kipindi hicho, kampeni hii itaenda kwa kibwagizo chenye msemo wa “Trash 4 Cash,” alisema.

Alisema faida ya kampeni hiyo ni kutoa ufahamu na uelimishaji wa uhifadhi na utunzaji endelevu wa mazingira kwa ujumla na kuunga mkono juhudi za serikali katika kujenga jamii bora yenye kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mzingingira na usimamizi endelevu wa mazingira.

Pia ukuzaji wa sekta ya utalii wa fukwe kwa kuwezesha utunzaji wa fukwe wa muda wote na kufanikisha mvuto wa fukwe kama sehemu mojawapo ya kipato cha taifa kupitia sekta ya utalii.

“Faida nyingine ni uwezeshaji wa kiuchumi na kifursa kwa vijana na wanawake kupitia mradi huu (mchanga pekee) na kupunguza ongezeko la chupa za plastiki katika jamii na kufundisha jamii njia bora za uhifadhi na ubadilishi bora wa matumizi ya chupa za plastiki,” alisema.

Alisema lengo jingine ni kutoa ulinzi na uhifadhi wa ekolojia ya viumbe vya baharini na nchi kavu.

Mwishoni mwa mwaka jana, Shirika la International Council of Beverages (ICBA) lilitoa ripoti inayoonesha uchafuzi wa fukwe umefikia wastani wa vipande vya plastiki 13,000 kwa kilometa mbili za fukwe za baharini.

Utafiti huo umebaini kuwa kuna tani milioni 150 za plastiki kwenye fukwe duniani mpaka sasa.

Comments

Comments are closed.

More in Top Stories