Alexis Sanchez ana matumaini ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa na Manchester United.
United itaikabili Paris Saint-Germain kwenye hatua ya 16 bora katika Uwanja wa Old Trafford Jumanne hii huku ikiwa na matumaini kibao baada ya kushinda mechi 10 kati ya 11 kwenye mashindano yote chini ya Ole Gunnar Solskjaer na ikitoka kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Fulham.
Sanchez alikosa taji la Ligi ya Mabingwa akiwa na Barcelona, baada ya kujiunga na klabu hiyo ikiwa imetoka kushinda taji hilo mwaka 2011, kisha akaondoka na kujiunga na Arsenal na Barcelona wakashinda tena taji hilo mwaka 2015.
“Ligi ya Mabingwa Ulaya ni ndoto ya kila mwanasoka,” alisema Sanchez alipozungumnza na Sunday Mirror.
“Nimeishi kwenye ndoto hii Barcelona na kuona inakuwaje. Nina matumaini ya kushinda taji hili hapa na sio sababu kwanini tusishinde.
“Tumevuka hatua ya makundi na mechi ijayo tunacheza na PSG. Ni mechi ngumu lakini ina dakika 180-lolote linaweza kutokea.
“United ni klabu yenye historia kubwa na ina uwezo wa kumfunga yoyote. “Kama tukishinda Old Trafford na tusiporuhusu wavu wetu kuguswa, basi tunatakuwa na nafasi nzuri kwenye mchezo wa marudiano.
“Nadhani tunaweza kufanya hilo na naiona United hii ina nafasi kubwa ya kupata bao Paris.”
Comments