Kamati ya mashindano ya Chama cha soka Mkoa Manyara (MARFA) imezifungia timu mbili zilizojaribu kupanga matokeo kwa muda wa miaka mitatu na faini ya Sh 500,000.
Timu za Fire Stone ya kiteto na Morning Star ya mbulu, zimefungiwa na kushiriki michuano yoyote kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya kubainika kupanga matokeo kwenye Ligi ya Daraja la tatu ngazi ya mkoa.
Timu hizo pia zimepigwa faini ya Sh 500,000 kwa kila timu kutokana na kupanga matokeo katika mchezo wa Ligi Daraja la tatu ngazi ya mkoa wa Manyara katika hatua ya sita bora.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Katibu Mkuu wa Kamati ya MARFA, Yusuph Mdoe, alisema wameamua kuzifungia timu hizo ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema kwamba timu zinatakiwa kufanya maandalizi yakutosha ili kuhakikisha zinaleta upinzani na mshindi apatikane kwa halali.
“Tumezifungia timu mbili kujihusisha na michezo kwa kipindi cha miaka mitati ambapo pia kila moja itatoa faini ya Sh. 500,000 ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema Mdoe.
Alisema wanatarajia kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali baadhi ya viongozi wa timu hizo ambao walijihusisha kwa namna moja au nyingine katika upangaji wa matokeo.
Mdoe alisema kuna baadhi ya viongozi wanaotumia vibaya madaraka kutokana na kuzisaidiatimu zao kupanga matokeo kitu ambacho ni kinyume na taratibu na kwamba hawatawavumilia ili kuhakikisha mchezo huo unachezwa kwa kufuata kanuni.
Comments