Makala

Mradi wa Pasipoti ya Kielektroniki pamoja Faida zake

0
Mradi wa Pasipoti ya Kielektroniki pamoja Faida zake
Passport ya Kielektroniki Tanzania

Pasipoti ni hati inayotolewa na Serikali ili kuthibitisha anayemiliki ni raia wake kwa madhumuni ya kusafiri katika nchi za nje na ikiomba atambuliwe kama raia wake.

Serikali ya Tanzania inatoa aina tofauti za hati ya kusafiria kwa raia wake kutokana na sheria ya mwaka 2002, na utekelezaji wake wa mwaka 2004.

Chombo pekee kilichopewa mamlaka ya kusimamia shughuli ya utoaji wa hati za kusafiria ni Idara ya Uhamiaji Tanzania, chini ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji.

Hadi sasa hati za kusafiria zinapigwa chapa Makao Makuu ya Ofisi za Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam na Zanzibar.

Mradi wa Uhamiaji Mtandao ulizinduliwa rasmi na Rais Dk. John Magufuli Januari 31 mwaka huu mara baada ya uzinduzi huo, hati mpya za kielektroniki zilianza kutolewa.

Hati hizo zilianza kutolewa Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu, Dar es Salaam na Ofisi Kuu ya Uhamiaji, Zanzibar.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Evalist Ndikilo, ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Pwani, amesema lengo la kuanzishwa kwa hati mpya ya Kielektroniki ya Afrika Mashariki ya Tanzania ni kukidhi matakwa ya usalama wa nchi.

Soma pia:  Jinsi ya Kupamba chumba cha kulala

Pia, kukidhi viwango vilivyopendekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Usafiri wa Anga.

Mhandisi Ndikilo anasema hati hizo zinatoa fursa ya utambulisho wa pamoja wa raia wa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki wanapokuwa nchi za nje.

Anasema hati mpya ya kusafiria ya kielektroniki itakuwa na manufaa mengi kwa wananchi na serikali.

Anataja faida za hati hiyo kuwa imetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa (chipu) yenye uwezo wa kubeba taarifa mbalimbali za muombaji pamoja na alama nyingine za kiusalama ambayo ni vigumu kugushiwa.

Faida nyingine ni kumuwezesha mtumiaji kupita katika sehemu zilizofungwa vifaa maalumu vya utambulisho na kuepuka msongamano wa foleni ya kusubiri huduma isiyo na ulazima awapo safarini.

Pia, itamuwezesha mtumiaji kuwa na nakala ya hati hiyo kwenye simu yake kiganjani itakayojulikana kama Emergency Electronic Passport baada ya kupakua ‘App’ ya hati yake kwenye simu.

Soma pia:  Top 10 ya Nchi tajiri Afrika kwa GDP

“Hii itamuwezesha mtumiaji kupata huduma ya haraka katika balozi za nje ya nchi, pale inapotokea amepoteza hati yake,” anasema.

Kuhusu utaratibu wa utoaji wa hati hiyo mpya, anasema itamlazimu muombaji kuwasilisha kitambulisho chake cha taifa kama sharti muhimu.

Mhandisi Ndikilo anasema hati za kusafiria za kawaida zitaendelea kutumika hadi Januari, mwaka 2020, kwamba baada ya hapo zitaondolewa kabisa kwenye matumizi.

Anataja gharama halisi ya hati ya Kielektroniki ni TZS. 150,000/- kama ambavyo Rais Dk. Magufuli alisisitiza wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Uhamiaji Mtandao.

Hata hivyo, anasema hati ya kusafiria ya Afrika Mashariki ilivyokuwa ikitumika awali, haitatolewa kufuatia kuwepo kwa ya Kielektroniki ya Afrika Mashariki ya Tanzania amabayo ni ya kimataifa.

Alitoa rai kwa Watanzania watakaopata hati hiyo mpya kuzitunza vizuri ili zisiangukie mikononi mwa wahalifu.

Alitoa wito kwa watumishi wa Uhamiaji watakaotoa huduma hiyo kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa na kwa kuzingatia sheria ya pasipoti na hati ya kusafiria ya mwaka 2002.

Anasema mtu ambaye atapoteza pasipoti yake kwa mara ya kwanza itamgharimu kulipa TZS. 500,000/- na mara ya pili TZS 750,000/-.

Soma pia:  CAG azua jambo Tabora

Kamishna wa Uhamiaji Raia na Pasipoti, Gerald Kihinga, anasema tangu ulipozinduliwa mradi huo Idara ya Uhamiaji tayari imeshatoa pasipoti za kielektroniki 15,101.

Akitaja mchanganuo wa pasipoti hizo za kawaida ni 14,818 za utumishi 44, kidiplomasia ni 234 na pasipoti maalumu za kidiplomasia tano.

Anasema mfumo huo utasaidia kuboresha usimamizi wa utoaji wa vibali kwani mwombaji atawasilisha maombi yake kwa njia ya kielektroniki.

Kamishna huyo anasema mfumo huo utasaidia kukuza sekta ya uwekezaji nchini kwa maendeleo ya uchumi nchini.

“Kwasasa tumeanza kufunga mfumo wa utoaji huduma hzizi mikoani, ambako awali tumeshaanza kutoa huduma hii katika jiji la Dodoma na tayari huduma hiyo imeanza kupatikana ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema.

Nitasimamia kazi hiyo kwa uadilifu wa hali ya juu na mtu yoyote ambaye atakuja kupata huduma hii na kukutana na changamoti ambayo itamletea vikwazo asisite kutoa taarifa,” alisema.

Comments

Comments are closed.

More in Makala