Kuna mengi ya kuyaona ukiwa nchini Cuba. Inategemea muda ulionao. Hata hivyo, nilipotembelea nchi hiyo nilijitahidi kuona na kujifunza machache, hasa yale yanayokumbusha historia ya nchi hii na uhusiano wake wa kimataifa.
Nilifanya hivyo nilipotembelea makumbusho ya mapinduzi (Museo de la Revolución) katika mji mkongwe wa Havana. Ukiwa hapo unaweza kuona jinsi nchi hii ilivyofanikiwa kuuondoa utawala wa kidikteta na kuleta maendeleo ya kijamii.
Makumbusho yenyewe yamo katika jengo la kifahari lililokuwa kasri ya mtawala, Fulgencio Batista kabla ya kupinduliwa.
Mlangoni utakuta Fidel Castro amenukuliwa akisema kabla ya mapinduzi alikuwa akilichukia jengo hilo kama makazi ya dikteta.
Hata hivyo, baada ya wananchi kulichukua sasa limegeuka darasa la kujifunza historia ya mapinduzi. Na ndio maana ukiwa hapo utakutana siyo tu na wageni kutoka kote duniani wanaotaka kujua historia ya Cuba, bali wanafunzi wa shule wanaonekana wakiwa na kalamu na madaftari wakitaka kujua yale yaliyofanyika kabla hawajazaliwa.
Na ndani ya makumbusho utaona jinsi tarehe 1 Januari 1959 (miaka 60 iliyopita) dikteta Batista alivyopanda ndege na kutoroka baada ya mapigano ya Santa Clara.
Kikosi kilichoongozwa na Che Guevara kiliingia mjini na kuipindua treni iliyokuwa imebeba askari wa Batista.
Na tarehe 7, Januari wanamapinduzi 9,000 wakiongozwa na akina Castro, Che na Camilo Centfuegos waliingia mji mkuu wa Havana wakishangiliwa na maelfu ya wananchi.
Hawa ni wanaukombozi waliopewa jina la vuguvugu la 26 Julai (26th of July Movement).
Ripoti ya kijasusi ya CIA ilisema Castro aliungwa mkono na wananchi wa Cuba, hasa wavuja jasho. Hii ilitokana na sera yake ya kuinua hali yao ya maisha na hivyo kuwafanya wazidi kumuunga mkono.
Majasusi wa CIA walijaribu zaidi ya mara 600 kumuua Castro lakini walishindwa. Waliojaribu kumuua walitangulia wao naye aliishi hadi umri wa miaka 90 na akafariki mwaka 2016 kwa ugonjwa na siyo kuuawa.
Mnamo Aprili 1961 majeshi ya CIA yalishambulia Cuba na tunaona jinsi wananchi walivyojitolea kuilinda nchi yao.
Mapigano hayo ya Playa Giron (maarufu kama Ghuba ya Nguruwe au Bay of Pigs) yalichukua muda wa saa 72 tu na wavamizi wakatokomezwa.
Utaona jinsi mnamo 1960 vijana 300,000 walivyojitolea kuishi na wakulima vijijini na kuwafundisha jinsi ya kusoma na kuandika. Katika muda wa mwaka mmoja kila mwananchi wa Cuba aliweza kusoma na kuandika.
Aidha vijana walijenga shule 37 katika muda huo, tofauti na miaka 57 kabla ya mapinduzi ilijengwa shule moja tu.
Mwananchi wa Afrika anayetembelea Cuba hawezi kukosa kuona kumbukumbu ya vijana 385,908 wa Cuba waliojitolea kwenda kusaidia ukombozi wa Angola iliyokuwa ikitawaliwa na Wareno wakisaidiwa na wenzao makaburu wa Afrika Kusini.
Mnamo 1983 vijana hao walikusanyika mbele ya ofisi ya majeshi iliyo katika uwanja wa mapinduzi (Plaza de la Revolución) jijini Havana. Wengi walifika alfajiri ili wawahi kujiandikisha kwenda Angola kama askari wa kujitolea. Katika uwanja wa mapambano Wacuba 2,398 walijitoa mhanga roho zao.
Wakiwa Angola mapambano makali yalifanyika katika mji wa Cangamba kuanzia tarehe 2 hadi 10 Agosti 1983.
Wapiganaji wa chama cha ukombozi wa Angola (People’s Armed Forces of Liberation of Angola au FAPLA) wakisaidiwa na wenzao kutoka Cuba waliwashinda makaburu.
Nchini Cuba wananchi wanakumbushwa jinsi vijana wao waliokwenda kupigana Angola walivyoshirikiana na vijana wa Angola na kumshinda adui.
Siku chache kabla ya hapo makaburu walitamba kuwa hawatashindwa. Badala yake walifyata mkia na kujinusuru kutoka katika kipigo kikali.
Mapigano ya Kifangondo, Cangamba na Cuito Cuanavale yatakumbukwa katika historia ya Cuba na Afrika.
Ni Cuito Cuanavale ndiko makaburu walipata kipigo cha mwisho kilichoashiria kuporomoka kwa utawalaa wa makaburu nchini Angola na Afrika Kusini kwa ujumla.
Ukiacha ukombozi wa Angola, kuna maelfu ya walimu, madaktari, wahandisi na wajenzi kutoka Cuba ambao wamejitolea katika bara la Afrika.
Tarehe 23 Mei 1963, kwa mfano ndege ya Cuba (Cubana de Aviación) ikiwa na madaktari 33, wauguzi 14 na wataalamu wa maabara saba iliwasili Algeria. Huu ulikuwa msafara wa kwanza wa wataalamu wa Cuba kuja kusaidia Afrika.
Baada ya hapo uhusiano huu wa Cuba na Afrika ulikuwa kwa haraka na zaidi ya Waafrika 34,000 walipelekwa Cuba kujifunza fani mbali mbali katika vyuo vikuu vya Cuba.
Kikosi cha Cuba chenye wapiganaji 865 wakiwa na silaha kamili waliwasili Angola kati ya tarehe 21 na 29 Oktoba 1963. Baada ya hapo kikafuata kikosi cha madaktari.
Huu ni mwanzo wa Operesheni Carlota iliyoanza mwaka 1975 hadi 1991. Carlota ni jina la mtumwa mwanamke wa Kiafrika aliyewaongoza wenzake waliopigana dhidi ya utumwa nchini Cuba mwaka 1843.
Leo katika jimbo la Matanzas (Cuba) kuna makumbusho kuhusu mama huyu kabila la Yoruba aliyepigania uhuru wa watumwa katika shamba la miwa.
Operesheni hii ni matokeo ya ombi la kiongozi wa MPLA, Dk Agostinho Neto kwa Rais Castro wa Cuba. Aliomba msaada wa kijeshi kwa vile majeshi ya makaburu kutoka Afrika Kusini yaliingia Angola kuwalinda wakoloni wa Kireno waliokuwa wameelemewa na wapiganaji wa MPLA.
Vijana wa Cuba walijitolea pia kwenda Ethiopia mwaka 1978 baada ya nchi hiyo kushambuliwa na waasi kutoka Somalia.
Hii ni Oparesheni Baragua iliyomalizikia mwaka 1989 na jumla ya Wacuba 41,730 walishiriki. Katika operesheni zote barani Afrika jumla ya vijana 2,398 kutoka Cuba walipoteza maisha yao.
Wacuba walifanya yote haya si kwa sababu walitegemea kupata chochote kutoka Afrika. Walikuwa wakitimiza wajibu wa mwanaharakati mmoja kumsaidia mwanaharakati mwenzake popote alipo duniani.
Hii ndiyo falsafa ya mapinduzi ya Cuba ambayo iliwaongoza vijana waliojitolea kwenda Afrika kushiriki katika ukombozi wa bara hili na katika matibabu ya wananchi wake.
Vijana hawa walijifunza kutoka mapinduzi ya Cuba. Wengi wao walikuwa hata hawajazaliwa wakati kina Castro na Che walipokuwa wakipigana katika milima ya Sierra Maestra, Playa Girón, Moncada na Granma. Leo maadui wanatumia mtandao wa Facebook ili kuwafanya vijana wasahau haya lakini nchini Cuba mtandao huo unaitwa Fakebook.
Ndio maana mwaka 1983 walijipanga kwa maelfu ili kujiandikisha kwenda Afrika. Leo ukitembelea makumbusho za Cuba utayaona haya. Na ndio maana wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanafika hapo ili wajifunze historia ya Cuba.
Wacuba wanajifunza jinsi nchi yao ilivyounga mkono ukombozi siyo tu wa Angola bali bara zima la Afrika. Cuba ililaani utawala wa makaburu Afrika Kusini na ikadai utawala huo umwachie huru Nelson Mandela. Na makaburu hao walipoivamia Angola vijana wa Cuba waliungana na MPLA kuwatokomeza wavamizi hao.
Cuba pia iliwalaani makaburu walioivamia na kuikalia Namibia. Mwaka 1988 Cuba ilikubali kuondoka Angola kwa masharti kuwa na makaburu nao waondoke Namibia.
Makaburu walilazimika kuondoka Namibia, kwani hawakutaka Cuito Cuanavale nyingine nchini Namibia.
Viongozi wa Cuba walilichukulia suala la msaada kwa Afrika kama kulipa deni la kihistoria ambalo Afrika inaidai Cuba. Castro alikuwa siku zote akikumbusha uhusiano wa kistoria baina ya Cuba na Afrika kwa vile wananchi wa Cuba wamechanganya damu ya Afrika.
Naye mchungaji, Abbuno Gonzalez wa kanisa la Pentekosti nchini Cuba alitilia mkazo kwa kusema, “Mababu na mabibi zangu waliletwa hapa kutoka Angola.
Kwa hiyo ni wajibu wangu kwenda kuwasaidia ndugu zangu wa huko. Hilo ni deni la mababu zangu ambalo nalilipa.”
Mwezi wa Julai 1991 Nelson Mandela alipotembelea Cuba alikumbusha mchango wa nchi hiyo kwa Afrika.
Akitaja mapambano ya Cuito Cuanavale, alisema: “Sisi Waafrika tumeona wageni wakija katika bara letu na kutugawa katika makoloni, kututawala, kutunyonya na kutugeuza watumwa.
Ni nadra kuona wageni wakija kutusaidia katika vita vya ukombozi na kutoa mhanga roho zao.
Cuba ni mfano bora, kwani bila ya ushindi wa Cuito Cuanavale dhidi ya makaburu ukombozi wa Afrika Kusini ungechelewa na mimi nisingepata bahati hii ya kutembelea Cuba.”
Yeyote anayetembelea Cuba leo anaweza kuona historia hii ya Cuba na jinsi mapinduzi yake yalivyosaidia ukombozi wa Afrika. Ndipo nilipokuwa huko nilijiuliza – hivi sisi Waafrika tunayakumbuka haya au tunajaribu kuyasahau?
Comments